Post by Yona Maro on Nov 18, 2005 3:20:29 GMT -5
Nimemaliza kusoma barua ya msomaji ambaye simtaji jina maana hajaniruhusu. Nimeibandika barua yake hapo chini. Nimetoa sentensi mbili za mwanzo wa barua ambazo zilikuwa ni salamu. Vingine vyote nimeviacha. Soma kwa makini anayosema. Kama hupendi kutazama mambo kwa mapana na marefu unaweza kudhani anayosema ni porojo au ndoto za Alinacha (hivi Alinacha aliota nini tena?). Haya, msome huyu bwana:
Kwako ndugu Ndesanjo,
Mada yangu mahsusi katika barua hii ni kuhusu mchakato mzima wa suala la uchaguzi Zanzibar.Nadhani yaliyotokea umeyapata na ikiwa hujayapata nitakupa kwa ufupi tu kwa kukuona wewe ni mwanamapinduzi halisi wa fikra.Ndesanjo tumepata pigo sisi wana demokrasia wa hapa Tanzania na jibu nililolipata ni kuwa hapa Tanzania hakuna demokrasia.Demokrasia ya viongozi wa Bongo ni chuki,kutiana vilema na mauaji.Ukitaka kuyajua haya fuatilia uchaguzi wa Zanzibar.
Ndesanjo, hakuna shaka upinzani umeshinda uchaguzi Zanzibar lakini je nani anaweza kuwakabidhi nchi?Zanzibar ilikuwa kama Iraq kwa muda wa siku nne,watu waliwekwa chini ya ulinzi wa wanajeshi ambao kazi yao ni kulinda mipaka sasa wanatumika kutisha na kuua raia wanaowalinda.Hii ni aibu kwa serikali ya Tanzania,kumbe haitaki kuondolewa madarakani kwa njia ya kura.Sio siri hakuna Mtanzania mwenye akili iliyochujwa ambae anaikubali hii serikali yetu kwani sasa sote tunajua kumbe nchi hii inatawaliwa kijeshi.
Sisi watu wa Tanzania bara tumekata tamaa kabisa ya uchaguzi kwa kuona yale yaliyotokea Zanzibar.Tulikuwa na muamko wa kuiondoa hii serikali ya CCM kwa njia ya kura lakini hili tumeona halitawezekana.Nashangaa sana vikosi vyetu vya majeshi vinakubali kuua na kutesa raia ambao pia ni ndugu zao kwa maslahi ya wachache.Hawa viongozi hawajui kwamba hii mbegu wanayoipanda hivi sasa ni mbaya sana?Hivi binadamu gani atakaekubali kuonewa kila siku?Ipo siku hali ya hapa Tanzania haitatofautiana na Jamhuri ya Congo,Somalia,Iraq na kwingineko ambako huko kote hakukaliki kwa ajili ya viongozi wenye tamaa.
Tunasikitika serikali ya CCM hapa Tanzania imeweza kuwatisha mpaka waangalizi wa uchaguzi wa kutoka nje ya nchi ambao kwa kweli nao wamekubali vitisho vyao na kutoa taarifa za uongo eti kweli uchaguzi ulikuwa huru na haki.Mkapa ndie aliewatisha mpaka wamesahau majukumu ya kazi yao.Ndio hapa nauliza nini maana ya demokrasia?
Tunashukuru tu kuwa Marekani imeona yenyewe na kutamka kuwa uchaguzi wa Zanzibar ni hovyo japo katika hili hatujui nayo itasimamia upande gani kutokana na yenyewe kuwa na sera kama za CCM.Kama kweli wana dhati basi wanaweza kuzuia umwagikaji mkubwa wa damu huku Tanzania kwani Watanzania wameshachoka na ubabe wa CCM.
Ndesanjo muda haunitoshi tu wewe si unajua haya maisha ya Bongo nimejinyima kula ili nikuandikie wewe hii barua huku kutuma Email ni shilingi 500/=
Mtiifu.
X.
ndesanjo macha